HIVI SASA NI SAA

TAREHE

Monday, May 23, 2011

Ushahidi wa Asili ya lugha duniani







Lugha zote duniani - tangu Kiingereza hadi Mandarin - chimbuko lake ni barani Afrika tangu makumi ya maelfu ya miaka iliyopita, utafiti umeonesha.
Baada ya kutafiti lugha zipatazo 500, Dr. Quentin Atkinson, mtaalamu wa masuala ya Lugha, amegundua ushahidi wa kutosha kwamba lugha zote duniani zilianzia Afrika toka katika jamii za babu na bibi zetu walioshi katika Zama za Mawe (Stone Age)
Utafiti huu si kwamba unaonesha tu kuwa lugha zimeanzia Afrika bali pia unaonesha kwamba lugha au matamshi yalitumika na mwanadamu tangu miaka zaidi ya 100,000 (laki moja) iliyopita, zamani ikifikiriwa kuwa ilikuwa ni pungufu ya hapo.
Wataalamu wa masuala ya mageuzi endelevu (evolution) wamezipokea habari hizi kwa nderemo na vifijo wakisema huu ni ushahidi mwingine kwamba binadamu amekuwa akiboresha maisha yake siku hadi siku. Kwa sasa upo ushahidi kwamba mwanadamu wa kwanza alitembea katika uso wa dunia kati ya miaka laki 2 au laki moja na nusu iliyopita na kwamba miaka elfu sabini baadae binadamu walianza kuhama toka kwenye bara la Afrika na kwenda sehemu zingine za dunia.
Japo wanasayani wanao ushahidi wa kutosha kuhusu kuhama huku kwa binadamu lakini bado hawana uhakika kwamba ni wakati gani hasa binadamu alianza kutumia lugha kuwasiliana. Wapo wanasayansi wanaosema lugha ziliibuka nyakati tofauti na pia wapo wanaosema lugha zote ni matawi toka kwenye lugha moja ya awali.
Dr. Atkinson wa Chuo Kikuu cha Auckland, amegundua ushahidi mkubwa unaoonesha kwamba lugha zote duniani ni matawi ya lugha ya awali ya Afrika. Katika utafiti wake aliouchapisha katika jarida la Science, amehesabu aina za sauti zilizoko kwenye lugha zisizopungua 504 na kuzipanga katika jedwali.
Anasema, Kiingereza, kwa mfano, kina sauti zipatazo 45, wakati lugha za Amerika ya Kusini zina sauti zisizozidi 15, na wakati huohuo jamii ya Bushmen kama Wasandawe wa Tanzania na Khoisan wa Botswana lugha zao zina sauti zaidi ya 200.
Dr. Atkinson anasema idadi ya sauti ni kielelezo kikubwa kwamba ni kwa jinsi gani lugha husika imeathiriwa zaidi na lugha za kusini mwa bara la Afrika. Anaendelea kusema kwamba tofauti ya idadi ya sauti unatokana na jinsi watu walivyokuwa wakihama tangu miaka elfu sabini iliyopita. Lugha zinabadilika (kukua au kufa) kutokana na kurithishwa toka kizazi kimoja hadi kingine.
Katika jamii zenye idadi kubwa ya watu lugha ina nafasi kubwa ya kuishi kwa muda mrefu na kukuza misamiati yake kwa sababu kizazi kipya kinakuwa kinayo kumbukumbu ya misamiati iliyokuwa ikitumia na kizazi kilichopita.
Lakini jamii yenye idadi ndogo ya watu na ambao bado wataendelea kuhama a hivyo kuzidi kupunguza idadi yao, lugha ina uwezo mkubwa wa kupteza sauti zake za awali na hata kufa kabisa wakati mwingine toka kizazi kimoja hata kingine.
Profesa Mark pagel, mtaalamu wa sayansi ya Bailojia, anasema kuwa ubadilikaji wa lugha unaonekana pia hata katika sayansi ya DNA. Profesa anasema jinsi unavyozidi kwenda mbali na Afrika ndivyo jinsi unavyozidi kupoteza sauti za asili za lugha yako.
Afrika tunao mchango mkubwa sana katika historia ya maisha ya mwandamu, cha ajabu tunaacha yetu yaliyo mema na kuiga ya wenzetu ambao walifanya tu kuhama toka hapa na kwenda sehemu nyingine duniani. Wao wanatazama Afrika kujifunza lakini wakati mwingi wanakuta tunafanya yale wanayofanya wao, na kwa bahati mbaya hatuigi ya maana, tunafata ya kishenzi tukidhani ndio usasa. Afrika Amka Sasa!

No comments: