Habari zilizotufikia hivi
punde kutoka Jijini Arusha zinaarifu kuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini
Kati, Ask Thomas Laizer amefariki dunia.
Taarifa hizo zinadai kuwa
Ask. Laizer amefikwa na umauti alasiri ya leo katika Hospitali ya Rufaa ya
Selelian ya Mjini Arusha.
Jana Februari 6, 2013 Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, alimtembelea na
kumjulia hali Askofu Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Taarifa zilipasha kuwa
Askofu Laizer alilazwa Hospitalini hapo kwa zaidi ya mwezi mmoja, na hakuna
daktari wala ndugu aliye tayari kusema ugonjwa unaomsibu.
Pinda alikwenda hospitalini
hapo jana saa 9 alasiri na kukaa zaidi ya nusu saa, huku waandishi wa habari
wakizuiwa kuingia katika chumba alimolazwa cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi
maalumu.
Hata hivyo, baada ya kutoka
katika chumba hicho kama ilivyo ada ya viongozi kuzungumzia hali ya mgonjwa,
Pinda hakuzungumza na waandishi wa habari na kulikuwa na ulinzi mkali ambapo
pia waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza naye.
SHP Blog inatoa pole kwa
Waumini na washarika wote wa KKKT nchini kote kufuatia msiba huo mzito
ulilolikumba Kanisa la Kilutheri hasa wakati huu ambao kuna mgongano kati ya
waumini na Viongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati.
No comments:
Post a Comment