HIVI SASA NI SAA

TAREHE

Wednesday, October 20, 2010

Una tatizo la kukosa usingizi?


Mtu mwenye afya nzuri, anahitaji kupata usingizi mzuri pia. Kuna baadhi ya watu hujaribu kulala lakini hawapati usingizi na wengine hulala na kupata usingizi, lakini hukatika katikati ya usiku na kubaki macho hadi kunapambazuka.
Sababu za mtu kukosa usingizi zinatofautiana kati ya mtu na mtu, inategemea na hali ya kiafya, kiakili, kimwili na kitabia ya mtu husika. Mtu anaweza kukosa usingizi kwa sababu ya kuwa na msongo wa mawazo au hofu juu ya jambo fulani au anaweza kukosa usingizi kutokana na matumizi ya dawa au dawa za kulevya, kahawa na ‘nikotini’. Inaweza pia kusababishwa na mazingira mabovu ya mtu anayolala.
Kwa mtu mwenye afya njema na asiye na matatizo yoyote, mwili unatakiwa upumzishwe kwa muda wa saa 7.5 au 8.5 kwa siku, na iwe usiku. Kuna baadhi ya watu usiku hawalali na badala yake hulala mchana kutwa, tabia hii kiafya haikubaliki kwa sababu inaenda kinyume na utendaji kazi wa mwili kiasili.

DONDOO 10 ZA KUKUSAIDIA KUPATA USINGIZI
  • Kwanza ni lazima upange muda wa kulala na kumka ambao utaendana na ratiba yako, hakikisha unalala na kuamka katika muda huo huo ulioupanga bila kuzidisha wala kupunguza.
  • Kama una tatizo la kukosa usingizi, wakati unajiandaa kwenda kulala, usinywe vichangamsha mwili kama vile kahawa, pombe, sigara, chai nyeusi, n.k. Vitu hivyo huchangia kuvuruga usingizi.
  • Usifanye mazoezi muda mfupi kabla ya kwenda kulala. Kama ni mtu wa mazoezi na unakabiliwa na hili tatizo, fanya mazoezi yako angalau masaa 3 kabla ya kwenda kulala.
  • Hakikisha mazingira ya unapolala yanakuridhisha na yaliyotulia yasiyokuwa na makelele. Ni vizuri ukilala kwenye mazingira ya giza kuliko yenye taa na mwanga mkali.
  • Ukiwa na njaa na kiu, huwezi kupata usingizi mzuri. Aidha, inashauriwa kuepuka kula vyakula vigumu na kushiba kupita kiasi muda mfupi kabla ya kwenda kulala. Vile vile usile vitafunwa vyenye sukari sukari kabla ya kwenda kulala, huchangia kuvuruga usingizi kwani hupandisha kiwango cha sukari mwilini.
  • Inashauriwa kujisaidia kabisa kabla ya kwenda kulala, hupunguza uwezekano wa kubanwa na haja ndogo katikati ya usingizi na kulazimika kuamka ili kwenda kujisaidia.
  • Weka muziki laini na kwa sauti ya chini pembeni ya kitanda chako ili kukuliwaza na kutuliza ubongo wako.
  • Usomaji wa vitabu vya kiroho na kidini muda mfupi kabla ya kulala, hutuliza akili hivyo kukuwezesha kupata usingizi haraka. Usisome vitabu vya hadithi za kutisha au kusisimua muda mfupi kabla ya kulala, mambo huwa tofauti.
  • Kama wewe ni mnene kupita kiasi, punguza unene kwanza, kwani uzito ukizidi huchangia matatizo mengine ya kiafya, likiwemo la ukosefu wa usingizi. Unaposhituka kutoka usingizini, usiangalie saa, itakusababishia ‘mchecheto’, badala yake endelea kulala na kufumba macho, hatimaye utapitiwa na usingizi tena. Ushauri wa mwisho mwingine, kunywa vijiko viwili au kimoja kikubwa cha asali mbichi wakati unapanda kitandani!

No comments: